Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano shirikisho la vyuo vikuu mkoa wa Dar es salaam.
Mwenyekiti wa shirikisho hilo bwana Imani Matabula, amesema ufunguzi huo utafanyika katika viwanja vya chuo kikuu cha Dar es salaam, ambapo jumla ya vyuo 32 vimethibitisha kushiriki mashindano hayo.
Bwana Matabula amebainisha kuwa, shirikisho hilo limeandaa michezo ya aina tano ambayo ni mchezo wa mpira wa miguu (Football), mpira wa Pete (Netball), Volleyball, Basketball pamoja na mchezo wa kuogelea (Swimming).
Michezo hii inajumuisha vijana wa vyuo vikuu lengo likiwa ni kuwakutanisha vijana kutoka vyuo vikuu wenye vipaji tofauti tofauti kwa ajili ya kufahamiana na kurejesha fikra za wanavyuo katika mlengo mmoja ambao ulikuwa na milengo tofauti kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi uliofanyika October 2015, na kurejesha amani na mshikamano kwa vijana wote.
Mashindano hayo yataanza kesho tarehe 23 January, 2016 ambapo yatazinduliwa saa kumi jioni huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri mkuu wa nchini Mheshimiwa Kassim Majaliwa na kilele cha mashindano hayo ni January 30, 2016.