Itakumbukwa kuwa kwenye miaka kati ya 2005 na 2006, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi maarufu kama Albino, yalikuwa yakiripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari, na mengi yalikuwa yakitokea sehemu za machimbo kanda ya ziwa.
Hali hii ilimlazimu mwandishi nguli wa habari
mtanzania kutoka shirika la habari ya Uingereza kupitia idhaa yake ya Kiswahili
BBC – Swahili, kufanya utafiti wa kina, ili kupata ukweli ni kwa nini mauaji ya
ndugu zetu Albino yalikuwa yakitokea.
Baada ya ripoti yake kutangazwa, Tanzania na dunia
kwa ujumla iliingia kwenye msako mkubwa wa kuwakamata wahusika wa mauaji hayo.
Huko nchini Canada mchungaji mmoja ambaye pia mwenye Albinism anafahamika kwa
jina la Peter Ash, ilimlazimu kuja Tanzania kuangalia ni kwanini watu wenye
ulemavu wa ngozi wanauawa wakati ni binadamu kama walivyo binadamu wengine.
Rais wa Under The Same Sun Peter Ash.
Baada ya kurudi kwao Canada akaanzisha shirika la
Under The Same Sun mwaka 2008 na nchini Tanzania likasajiliwa mnamo mwaka 2009.
Kiukweli ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa
wakukumbana na changamoto nyingi, akizungumza na wanachuo kutoka chuo cha
ustawi wa jamii, clabu ya maafisa ustawi wanafunzi (Social work Club), Afisa
Utetezi wa Haki za Binadamu wa UTSS, bi Perpetua Senkoro, ambaye amepata bahati
ya kusomeshwa na shirika hilo na kumaliza shahada yake ya sheria chuo kikuu cha
Dar es Salaam, amebainisha changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni ile ya uoni
kutokana na macho yao kutokuwa na rangi yake ya asili (Melamine), ya kuweza
kuhimili mwanga mkali, na pia kwenye uoni wanatatizo la kitaalamu linafahamika
kama Nystagmus,
ambalo ni tatizo kushindwa
ku-control mienendo ya macho na yanabaki yakichezacheza.
Afisa utetezi wa haki za binadamu wa UTSS, bwana Kondo Seif, akiongea na wanachuo wa chuo cha ustawi wa jamii, hawapo pichani.
Changamoto nyingine ni kwenye suala la ngozi, pia
imekosa Melamine ambayo ni kinga dhidi ya mionzi ya jua, na kutokana na takwimu
mbalimbali, wakikosa mafuta tiba ambayo yanasadia kwenye ngozi zao wengi
hupatwa na kansa ya ngozi, kwani jua likiwapiga sana, mionzi ya jua husababisha
vidonda vinavyopelekea kupata kansa ya ngozi. Mafuta hayo ambayo huagizwa nje
ya nchi kama kipodozi na kutozwa kodi, yanauzwa bei ghali ambayo ni changamoto
kubwa kwao kumudu gharama za ununuzi, ingawa kuna baadhi ya hospitali huwa
yanapatikana lakini kwa uchache.
Changamoto nyingine ni ya usalama, hali ambayo
hushindwa kuchangamana na watu wengine kwa kuhofia usalama wao, iwe mchana au
usiku, kwani wamekuwa wakiwindwa na watu wenye imani hasi.
Afisa utetezi wa haki za binadamu wa Under The Same Sun, bi Perpetua Senkoro, akielezea changamoto wanazokumbana nazo watu wenye ulemavu wa ngozi.
Pamoja na changamoto hizo Afisa mwingine wa utetezi
wa haki za binadamu wa shirika hilo bwana Kondo Seif, ametoa rai kwa kila mmoja
kuwa balozi wa mwenzake pale wanapoona kuna mazingira hatarishi kwa ajili ya
ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, basi tushirikiane kuripoti matukio hayo.
Vile vile kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwa pamoja
tunaweza kuhamasishana katika kampeni ya kutokomeza mauaji ya albino, kwani
sote tunaishi kwenye dunia moja, tunategemea mwanga wa jua moja kwanini tuwaue
ndugu zetu ilhali nao ni binadamu na wana haki ya kuishi kama alivyo mwanadamu
mwingine?
Hata hivyo bwana Kondo, aliwaeleza wanachuo ambao ni
maafisa ustawi wa jamii watarajiwa kuwa, kuhusu suala la mafuta tiba, juhudi
zinaendelea kufanyika ili mafuta hayo yaingie kama dawa na si aina ya kipodozi
na tayari kuna tamko la serikali (declaration) lililoandaliwa kuwa MSD
wanapoagiza dawa zao na mafuta hayo yawe yanawekwa kwenye listi ya dawa na pia
kila afisa wa afya mkoa kuhakikisha kuna ugawaji wa mafuta hayo, na huenda
jitihada hizo zikasadia.
Vile vile kwa kuwa mafuta hayo yanaagizwa kutoka nje
ya nchi ambayo kidogo yana utofauti na hali halisi ya hewa na mazingira ya
kwetu, shirika la Kili Sun la mkoani Kilimanjaro, limeanza kutengeneza mafuta
hayo kulingana na hali halisi ya nchini kwetu, na juhudi zinaendelea ili
angalau ziweze kukidhi mahitaji ya wote.
Viongozi wa msafara wa wanachuo kwenye ofisi za UTSS kutoka kushoto ni Nurdin, Ally Ahmad na
James.
Picha za baadhi ya wanachuo waliotembelea ofisi za Under The Same Sun
Tushirikiane kwa pamoja katika kampeni ya kutokomeza mauaji ya Albino.